Rais Ruto apongeza wanariadha wa Kenya

Wanariadha hao walifanya vyema kwenye mashindano ya Silesia Diamond League nchini Poland Jumamosi.

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amepongeza wanariadha wa Kenya walioshiriki mashindano ya Silesia Diamond League nchini Poland ambapo Faith Kipyegon aliibuka mshindi wa mbio za mita elfu tatu kwa wanawake.

Kipyegon aliweka muda wa pili bora katika historia, akaweka rekodi mpya ya Afrika, ya Diamond League na kuongoza ulimwenguni kupitia mbio hizo hizo.

Kupitia mitandao ya kijamii kiongozi wa nchi aliandika, “Pongezi tena Faith Kipyegon kwa kushinda mbio za mita elfu 3 kwa wanawake katika mashindano ya Silesia Diamond League nchini Poland.”

Rais aliendelea kusema kwamba Kipyegon ameendelea kufafanua upya ukuu huku akihamasisha vizazi vijavyo.

Wanariadha wengine waliotajwa na Rais Ruto katika ujumbe wake ni pamoja Lilian Odira, ambaye aliweka muda bora wa kibinafsi katika mashindano ya mbio za mita mia 8 huku akiibuka nambari mbili.

Beatrice Chebet naye alinyakua nafasi ya pili katika mbio za mita 1500 sawia na Timothy Cheruiyo.

“Team Kenya mmepeperusha bendera yetu juu kwa mara nyingine, mmeinua fahari yetu na kuhakiki nafasi yetu ulimwenguni kama nchi yenye uwezo mkubwa katika michezo.” alimalizia Rais Ruto.

Share This Article