Rais William Ruto leo ameongoza maadhimisho ya siku ya jeshi la ulinzi la Kenya KDF katika kituo cha jeshi cha Moi huko Eldoret.
Katika hotuba yake kiongozi wa nchi alisema kwamba utayari wa jeshi kwa kazi unapimwa na uwezo wa wanajeshi hasa katika misingi ya uwezo wa kimwili, ustahimilivu kimawazo, maadili na usaidizi wa kijamii.
Rais alisema kutokana na ukweli huo, serikali imeweka vipaumbele vinne mihumu vya kuimarisha msingi wa jesji la ulinzi la Kenya, cha kwanza kikiwa maslahi ya wanajeshi na familia zao.
Hatua zilizochukuliwa kulinda maslahi ya wanajeshi ni pamoja na upanuzi wa taasisi za afya, ujenzi wa nyumba za makazi na uimarishaji wa mipango ya kuwasaidia.
Uwekezaji katika mafunzo na maendeleo ya kitaaluma ni suala jingine lililopatiwa kipaumbele na serikali, ambapo Rais alisema vifaa vya mafunzo vimeboreshwa, ujuzi wa kiteknolijia unatolewa na wanajeshi wanapata elimu faafu ya kitaaluma.
Usasishaji wa vifaa pia ulitajwa kama nambari tatu na Rais Ruto kwenye vipaumbele, ambapo alisema kwamba ujasiri pekee hauwezi kusaidia wanajeshi kushinda vita, lakini utayari unaweza.
“Serikali imeharakisha ununuzi na usasishaji wa mifumo ya ulinzi, imeboresha majukwaa ya usafiri na kuimarisha uwezo wa kimtandao na kijasusi” alisema Rais Ruto katika htuba yake.
Kipaumbele cha mwisho kulingana na Rais ni kuimarisha usaidizi wa kimawazo na kiroho, ambapo alisema kwamba mipango ya kushughulikia msongo wa mawazo, kujenga ustahimilivu na kutoa mwongozo wa maadili imewekwa.
Siku ya KDF huadhimishwa kila mwaka ili kutoa heshima kwa wanajeshi walioaga dunia wakiwa kazini na kusherehekea mchango wa wanajeshi kwa amani, usalama na maendeleo ya jamii.