Rais William Ruto ametuma risala za rambirambi kwa Rais wa Ghana John Mahama kufuatia ajali ya helipokta iliyotokea nchini humo jana Jumatano.
Watu wanane walithibitishwa kufariki kwenye ajali hiyo hiyo, wakiwemo mawaziri wawili.
“Tunatuma risala zetu za rambirambi kwa Rais John Mahama, serikali, watu wa Ghana na familia zilizopoteza jamaa wao kufuatia ajali ya helikopta iliyoua watu wanane, wakiwemo mawaziri wawili,” alisema Rais Ruto kwenye risala yake ya rambirambi.
“Tunasimama bega kwa bega na Ghana katika kuomboleza vifo hivi na kuwaombea walioathiriwa wakati huu wa huzuni.”
Waziri wa Ulinzi wa Ghana na mwenzake wa Mazingira pamoja na watu wengine sita, walithibitishwa kufariki baada ya helikopta walimokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la Ashanti.
Vifo vyao vilithibitishwa na msemaji wa serikali ya nchi hiyo.
Mawaziri Edward Omane Boamah wa Ulinzi na Ibrahim Murtala Muhammed wa Mazingira, Sayansi na Teknolojia walifariki kwenye ajali hiyo, huku Mkuu wa Wafanyakazi Julius Debrah akitaja ajali hiyo kuwa janga la taifa.
Awali, Vikosi vya Ulinzi vya Ghana vilisema kuwa helikopta aina ya Z9 iliyokuwa na wafanyakazi watatu na abiaria watano ilitoweka kwenye rada.
Helikopta hiyo iliondoka jijini Accra saa tatu na dakika 12 saa za nchi hiyo, ikielekea mjini Obuasi katika hafla ya kukabiliana na uchimbaji haramu wa madini.
Maafisa wa nchi hiyo bado hawajathibitisha chanzo cha ajali hiyo, huku Mkuu huyo wa wafanyakazi akiagiza bendera kupeperushwa nusu mlingoti.