Rais Ruto amwomboleza Munyao

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amemwomboleza aliyekuwa waziri na mbunge wa zamani wa eneo la Mbooni katika kaunti ya Makueni Joseph Munyao.

Kiongozi wa nchi alichapisha ujumbe wake kwenye akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii ambapo alisema taarif za kifo cha Munyao ni za kuhuzunisha.

“Tunatoa pole za dhati kwa watu wa familia yake na watu wa Mbooni kwa jumla, tunaposherehekea na kutoa heshima zetu kwa mtu ambaye alijitolea katika huduma.” Alisema Rais kwenye ujumbe wake.

Rais Ruto alikumbuka jinsi Munyao alishirikiana na wakulima ili kuboresha mapato yao, hatua ambayo anaitaja kuwa mchango mkubwa na wa kudumu kwa nchi hii.

Kulingana na Rais Ruto, utumishi wa Munyao katika sekta ya umma ulidhihirisha kujitolea na jukumu ambalo lilitoa mwelekeo kwa maisha ya wengi.

“Wapendwa wake na wakapate faraja katika ufahamu kwamba urithi wake ni stahimilivu katika jamii ambazo aliinua na nchi aliyoitumikia kwa heshima na kujitolea. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake katika amani ya milele.” Alimalizia Rais.

Kifo cha Munyao kiliripotiwa jana Jumamosi Novemba 22, 2025 akiwa na umri wa miaka 85.

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kabisa kama mbunge wa eneo la Mbooni mwaka 1975 kwenye uchaguzi mdogo ulioandaliwa kufuatia kupingwa kwa matokeo ya awali mahakamani.

Munyao alipoteza wadhifa huo kwa mara ya mwisho mwaka 2007 aliposhindwa na marehemu Mutula Kilonzo Senior.

Share This Article