Rais William Ruto amemwomboleza mwenyekiti wa Chama cha Taifa wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA) Johnson Nzioka akimtaja kama mtu aliyejitolea kupigania maslahi ya walimu wakuu humu nchini.
Nzioka alifariki jana Jumapili kupitia ajali iliyotokea kwenye barabara ya Mombasa Road.
“Johnson Nzioka alikuwa mtaalam wa elimu maarufu aliyepigania maslahi ya walimu wakuu katika nchi yetu,” amesema Rais Ruto katika mtandao wake wa X.
“Alikuwa na maono na alitumia muda wake mwingi kuwakuza wanafunzi waadilifu na wenye bidii. Maombi yetu yaiendee familia yake na familia ya KEPSHA.”
Waziri wa Elimu Julius Migos, Chama cha Walimu (KNUT) na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) ni miongoni mwa waliotuma risala za rambirambi kufuatia kifo cha Nzioka.
“Alikuwa mwalimu na kiongozi mwenye umaizi na aliyefanya kazi kwa kujitolea, aliyeutakia mfumo wetu wa elimu mema,” alisema Migos katika risala zake za rambirambi.
“Kama mwenyekiti wa KEPSHA, Nzioka alikuwa makini katika kuimarisha wajibu wa usimamizi wa shule ili kupata matokeo bora ya elimu.”
Katibu Mkuu wa KNUT Collins Oyuu amemwelezea marehemu kama kiongozi shupavu aliyekuwa na ujuzi wa kipekee wa kidiplomasia.
“Atakumbukwa kwa uzungumzaji wake wa unyenyekevu lakini wa wazi, hasa wakati wa kutafuta amani miongoni mwa wanachama wake,” alisema Oyuu.