Rais William Ruto amemuomboleza mwanamuziki wa nyimbo za injili Beatrice Wairimu Mbugua almaarufu Betty Bayo, akimtaja ambaye aliwapatia wakenya tumaini kupitia sauti yake.
“Kwa muda wa miaka 15, Betty aliwapa wengi matumaini kupitia nyimbo zake, zilizoashiria ukakamavu na kuwa na imani licha ya changamoto za maisha,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa nchi alisema jumbe katika nyimbo za Bayo, ziliahimiza kuto-kufa moyo bila kujali changamoto zilizopo.
“Sauti yake huenda imeondoka, lakini huduma yake itaendelea kuishi ndani ya nyoyo alizopatia tumaini.” aliongeza Rais Ruto.
Betty Bayo alifariki Jumatatu akipokea matibabu katika Hospitali Kuu ya Kenyatta.
Kifo chake kimetajwa kuwa huzuni kubwa kwa familia yake na jamii ya wanamuziki wa nyimbo za injili. Betty Bayo alijipatia umaarufu kwa nyimbo zake kama maneno ya kinywa changu na Eleventh Hour.