Rais William Ruto ameandaa dhifa ya staftahi mapema Alhamisi katika Ikulu ndogo ya Eldoret, kuwasherehekea washindi wa nishani za Olimpiki katika makala ya Paris yaliyokamilika Jumapili iliyopita.
Kenya ilimalzia ya 17 katika msimamo wa dunia kwa dhahabu 4 fedha 2 na shaba tano huku, ikiibuka bora barani Afrika katika mashindano hayo ya Olimpiki.
Ni mara ya kwanza kwa Rais Ruto kuwalaki wanariadha katika Ikulu ya Eldoret .
Beatrice Chebet alishinda dhahabu mbili katika mita 5,000 na 10,000 huku Faith Kipyegon akitwaa dhahabu ya mita 1,500 naye Emmanuel Wanyonyi katika mita 800.
Faith Kipyegon na Ronald Kwemoi walishinda medali za fedha katika mita 5,000 .
Faith Cherotich,Abraham Kibiwott,Hellen Obiri,Benson Kipruto na Mary Moraa walinyakua nishani za shaba.
Rais Ruto ameandamana na naibu wake Rigathi Gachagua na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula.