Rais Ruto akutana na viongozi wa Kisii Ikulu

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto leo Alhamisi amekutana na viongozi kutoka eneo la Kisii katika Ikulu ya Nairobi katika mkutano ambao pia ulihudhuriwa na kinara wa ODM Raila Odinga. 

Viongozi hao walijumuisha Gavana wa kaunti ya Kisii Arati Simba, Waziri wa Elimu Julius Ogamba na Mwanasheria Mkuu wa serikali Shadrack Mose.

Gavana Arati ni rafiki wa karibu wa Raila ambaye ameshirikiana na Rais Ruto kuunda serikali jumuishi.

Arati alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Kwa misingi hiyo, ziara hiyo inachukuliwa kama njama ya Rais Ruto na Raila kutumia viongozi hao, wanaoegemea upande wa serikali jumuishi, kupata uungwaji mkono wa eneo la Kisii kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Ikumbukwe kuwa viongozi wawili kutoka eneo la Kisii tayari wametangaza azima ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Wao ni Jaji Mkuu mstaafu David Maraga na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Taifa, Dkt. Fred Matiang’i.

Haijabainika ni kiasi gani cha uungwaji mkono ambao wawili hao watapata kutoka ngome yao ya kisiasa ikiwa watagombea urais.

Wabunge kadhaa kutoka eneo la Kisii, akiwemo Seneta Richard Onyonka na mbunge wa Kitutu Chache Kusini Anthony Kibagendi wameibuka kuwa wakosoaji wakali wa serikali ya Kenya Kwanza.

Lakini kitu kimoja ni dhahiri: kwamba eneo la Kisii litakuwa kitovu cha siasa kali katika uchaguzi mkuu ujao.

 

 

 

 

 

 

Share This Article