Rais Ruto akabidhi nyumba 1,080 za bei nafuu kwa wakazi wa Mukuru

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto akabidhi funguo 1,080 za nyumba za gharama nafuu kwa wakazi wa Mukuru,Nairobi.

Rais William Ruto leo Jumanne amekabidhi nyumba 1,080 za gharama nafuu kwa wakazi wa Mukuru Jijini Nairobi.

Nyumba hizo ni sehemu ya nyumba 13,248 zinazojengwa katika mtaa wa New Mukuru Housing, ambao utakuwa mtaa mkubwa zaidi katika historia ya Kenya.

“Hii ni siku muhimu sana katika safari yangu ya kisiasa. Tumekabidhi funguo 1,080 za nyumba. Katika nyumba hizi wakazi watapata usafi wa hali ya juu, usalama na kubadilisha maisha ya maelfu ya watu ambao hawangepata fursa hii,” alisema Rais Ruto katika mtaa wa Mukuru.

Huku akikabidhi familia hizo funguo, kiongozi huyo wa taifa alisema kuna miradi mingine zaidi ya 200 ambazo ziko katika viwango tofauti vya kukamilika na ambayo imetoa nafasi zaidi ya 200,000 za ajira kwa vijana.

“Tutaendelea kutoa maamuzi magumu na yenye ujasiri ambayo yatabadilisha taifa hili,” aliongeza kiongozi wa nchi.

Aidha Rais alitoa wito kwa wanasiasa kukomesha siasa zisizo na manufaa akisema serikali ya Kenya Kwanza inatilia mkazo utekelezaji wa ajenda ya maendeleo.

Aliwasuta wale wanaoendeleza kampeni za mapema akionya kwamba hawataruhusiwa kupinda azma ya serikali ya kutimiza ahadi yake kwa Wakenya.

Share This Article