Rais William Ruto amethibitisha tena dhamira ya serikali yake katika kufufua sekta ya kilimo kwa kukabidhi hundi ya thamani ya Shilingi bilioni 2.65 kwa Shirika la Maendeleo ya Majani Chai Nchini (KTDA).
Fedha hizo, ambazo awali zilikuwa amana katika benki zilizofilisika za Chase na Imperial, zilitolewa kupitia Shirika la Bima ya Amana ya Benki- KDIC na zinatarajiwa kuimarisha kwa kiwango kikubwa sekta ya chai nchini.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi hiyo katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto alisisitiza kuwa kilimo kimewekwa katikati ya ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi ya taifa.
“Tumeweka kilimo kama kiini cha ajenda yetu ya mageuzi ya kitaifa kwa sababu ndicho uti wa mgongo wa uchumi wetu, kikichangia karibu nusu ya Pato la Taifa, kuunda ajira kwa mamilioni, kuendesha biashara ya nje, na kuhakikisha usalama wa chakula” alisema.
Rais alielezea mageuzi kadhaa makubwa na ya kimkakati ambayo serikali yake imeanzisha kama usajili wa wakulima milioni 6.5, usambazaji wa magunia milioni 21 ya mbolea ya ruzuku, kuvunjwa kwa mitandao ya ulanguzi na kusafisha usimamizi wa sekta.
Alitaja pia kufunguliwa kwa masoko mapya ya kuuza nje na kuimarisha mifumo ya msaada katika mnyororo mzima wa kilimo.
Mageuzi haya, alisema, yameanza kuonyesha mafanikio, hasa katika sekta ya chai.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, bei ya chai imepanda kutoka wastani wa Shilingi 51 hadi Shilingi 64 kwa kilo, huku mapato ya mauzo ya nje yakiongezeka kutoka Shilingi bilioni 138 hadi Shilingi bilioni 250.
Hundi hiyo ya Shilingi bilioni 2.65 inatarajiwa kunufaisha maelfu ya wakulima wadogo wa chai wanaohusiana na KTDA, wengi wao wamekuwa wamekuwa wakingoja kwa muda mrefu kurejeshewa fedha zilizokwama katika benki zilizofilisika.
KTDA imetaja fedha hizo kuwa “afueni iliyochelewa sana” ambayo itasaidia kuimarisha shughuli za viwanda vya chai na kuongeza marupurupu ya wakulima.
Zitaelekezwa kwa viwanda vya chai husika ili kusaidia uwekezaji wa mtaji, uboreshaji wa miundombinu na utoaji bora wa huduma.