Rais William Ruto ametoa changamoto kwa timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars, akiitaka kujituma na kusajili matokeo bora wakati wa mashindano ya kombe la bara Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani – CHAN.
Makala hayo ya nane yataandaliwa kati ya Agosti 2 na 30 mwaka huu katika viwanja vitano vilivyoko katika miji mitano katika mataifa ya Zanzibar, Tanzania, Kenya na Uganda.
Harambee Stars itakuwa ikishiriki fainali za CHAN kwa mara ya kwanza.
Kenya imo kundi gumu la A pamoja na Angola, Zambia, Morocco na DR Congo.
Alipozuru kambi ya timu ya taifa siku ya Jumatano, Rais alielezea imani yake na uwezo wa wachezaji wa Harambee Stars kujituma na kuwapa Wakenya matokeo bora.
Timu hiyo chini ya kocha mkuu Benni McCarthy imepiga kambi ya mazoezi kujiandaa kwa kipute hicho.
Aidha, Ruto alitoa hakikisho la kutoa msaada wa hali na mali kwa Stars wakati wa kipute hicho.
Rais alikuwa akikagua ukarabati wa uwanja wa Kasarani ambao utaandaa mechi zote nne za Harambee Stars, na pia fainali ya kipute hicho.