Rais Ruto ahudhuria dhifa ya waanzilishi wa ODM

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto alihudhuria dhifa ya waanzilishi wa chama cha upinzani cha ODM huko Mombasa, hafla ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

Maadhimisho hayo muhimu ya chama cha ODM yanahusisha tamasha la siku tatu katika ukumbi wa Mama Ngina Waterfront na yalianza Ijumaa hadi leo Jumapili.

Wanachama wanasherehekea miongo miwili ta kile wanachokitaja kama miaka 20 ya huduma na harakati za kisiasa, huku wakiangazia pia urithi wa marehemu kiongozi wa ODM, Raila Amolo Odinga.

Uwepo wa Ruto katika hafla hiyo unaashiria maonyesho ya umoja wa kisiasa chini ya serikali jumuishi iliyo madarakani.

Ruto aliandamana na viongozi kadhaa waandamizi kutoka serikali yake, hatua inayoonyesha umuhimu anaozingatia katika hatua hii ya miaka 20 ya ODM.

Kwa mujibu wa ODM, maadhimisho haya si ya kawaida tu, pia yanatoa ujumbe kuhusu dhamira yake ya kutimiza ahadi kwa Wakenya.

Chama cha ODM kilibuniwa kwa misingi ya kampeni ya kura za maoni kuhusu mabadiliko ya katiba mwaka 2005 ambapo viongozi kama Raila Odinga, William Ruto, Musalia Mudavadi, Najib Balala na wengine walikuwa wakipinga mabadiliko hayo.

Walichagua alama ya chungwa kutumiwa kwa kura hizo za maoni huku waliokuwa wakiunga mkono mabadiliko hayo wakitumia alama ya ndizi.

Ulipofika wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2007, viongozi hao waliamua kubadili vuguvugu lao la chungwa kuwa chama cha kisiasa ambacho sasa kinafahamika kama ODM.

Share This Article