Rais Ruto ahimiza mabadiliko makubwa ulimwenguni

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amehimiza mabadiliko makubwa ulimwenguni hasa katika madeni na uungwaji mkono wa juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Kiongozi huyo wa Kenya aliyasema hayo katika mkutano kuhusu kuvunja mzunguko hatari wa madeni, mazingira na tabianchi jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Akihutubia viongozi wa dunia, Ruto alisema kuwa simulizi la Afrika kama mwathirika wa tabianchi sasa limepitwa na wakati. “Tumeandika upya simulizi hilo,” alisema.

“Afrika sasa ni kiongozi katika ukuaji chanya wa tabianchi, ikitoa suluhisho halisi kwa dunia iliyo kwenye ukingo wa hatari.” Aliendelea kusema Rais.

Alipongeza maendeleo yaliyopatikana tangu kongamano la kwanza kuhusu tabianchi barani Afrika la mwaka 2023 jijini Nairobi, ambapo bara la Afrika lilikumbatia kilimo kinachozingatia tabianchi, uendelezaji wa viwanda vya kijani na nishati safi kama nguzo za maendeleo mapya.

Hata hivyo, Ruto alionya kuwa ongezeko la madeni linaweza kuhujumu maendeleo hayo.

“Mwaka 2025 pekee, Afrika inakabiliwa na malipo ya madeni ya zaidi ya dola bilioni 90. Hii ni zaidi ya matumizi ya sekta ya afya au elimu katika nchi nyingi” alisema. “Hatuwezi kufadhili mustakabali wa kijani kwa bajeti zilizo nyekundu”.

Akinukuu ripoti mpya ya wataalamu iliyoongozwa na Kenya kwa ushirikiano na Columbia, Ufaransa na Ujerumani, Ruto alieleza mapendekezo 12 ya haraka ya kuunganisha mikakati ya tabianchi na madeni.

Inajumuisha kukuza uwekezaji wa kijani, kufungua mitaji binafsi na kudhibiti mtiririko haramu wa fedha.

“Msamaha wa deni si hisani, ni msingi wa ukuaji endelevu, jumuishi unaoendeshwa na ubunifu wa karne ya 21, si nishati za kale za karne ya 20” alisisitiza rais Ruto.

Alimalizia kwa kutoa changamoto kwa dunia akiitaka ivunje mzunguko hatari wa madeni na ianzishe mzunguko chanya wa ustawi kwa ajili ya Afrika na kwa ajili ya sayari.

Share This Article