Rais William Ruto Jumatatu jioni aliondoka hapa nchini kuelekea China, kwa ziara rasmi ya kiserikali.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili ulioanzishwa mwaka 2017, huku China ikiitambua Kenya kama mshirika mkuu katika ushirikiano wa uchukuzi barani Afrika.
Kenya imetekeleza wajibu mkubwa katika maendeleo ya miundombinu katika kanda hii, huku miradi kama vile Standard Gauge Railway na barabara ya Nairobi Expressway, ikiimarisha uchumi wa taifa hili.
Akiwa Jijini Beijing, Rais Ruto atashiriki mazungumzo na mwenzake Xi Jinping, kuimarisha mabadailiko ya kiuchumi, maendeleo endelevu na ushirikiano wa kimataifa.
Kiongozi wa taifa pia ataongoza mkutano wa kibiashara kati ya China na Kenya, utakaozileta pamoja zaidi ya kampuni 100 kutoka nchi hizo mbili, kwa lengo la kutafuta fursa mpya za kibiashara, uwekezaji, uvumbuzi wa dijitali na viwanda.
Akizungumza wakati wa mahojiano na China Media Group siku ya Jumamosi, Rais Ruto alisema anatazamia kuendeleza uhusiano kati ya wananchi wa mataifa haya mawili ambao umekuwepo kwa miaka mingi, ili kuongeza kasi mpya katika maendeleo ya uhusiano baina ya nchi hizi mbili.