Rais Ruto aelezea ufanisi katika sekta ya kilimo

Tom Mathinji
2 Min Read

Rais William Ruto amesema taifa hili limepiga hatua kubwa katika sekta ya kilimo, tangu serikali yake ilipochukua hatamu za uongozi.

Rais alisema mapato kutokana na mauzo ya Majani Chai yameongezeka kutoka shilingi bilioni 138 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 215 mwaka 2024.

Kiongozi wa taifa aliongeza kuwa sekta ya kahawa nayo ambayo ilikuwa katika hatari ya kusamnbaratika, inazidi kuimarika huku bei ya kilo moja ya kahawa ikiongezeka kutoka shilingi 70 hadi kati ya shilingi 120 na 150 kwa kilo.

Akizungumza alipokuwa akihutubia taifa kwenye majengo ya bunge, Rais Ruto alisema serikali imepanua ukuzaji wa bidhaa za kutengeneza mafuta ya kupikia kwa asilimia 90 katika mwaka 2022 na mwezi Aprili mwaka 2025.

Kulingana na Rais, hatua hiyo imepunguza uagizaji mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi kwa shilingi bilioni 17 katika muda wa mwaka mmoja.

Aidha, kiongozi wa taifa alisema sekta ya sukari ambayo awali ilikumbwa na misukosuko, sasa inaendelea kuimarika huku ardhi ya ukuzaji miwa ikiongezeka kwa ekari 200,000, huku uzalishaji wa miwa ukiongezeka hadi metrik tani 815,000 na uagizaji sukari kutoka nje ukipungua kwa asilimia 70.

Sekta ya mifugo haikuachwa nyuma, huku rais akisema uuzaji ngozi nje ya nchi umeongezeka kwa asilimia 56 hadi shilingi bilioni 2.5. Uuzaji wa nyama nje ya nchi pia alisema umeimarika kwa asilimia 45 hadi shilingi bilioni 12.9.

“Mageuzi haya ndiyo tuliyaahidi, na sasa yanatekelezwa kote nchini,” alisema Rais Ruto.

Kulingana na katiba ya Kenya Rais anapaswa kuhutubia taifa kwenye majaengo ya nchi kuelezea hali ya taifa ilivyo.

Share This Article