Rais Ruto adhihirisha imani ya kujenga kanisa jipya Ikulu

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto anaonekana kushikilia imani kwamba hatimaye atafanikiwa kujenga kanisa katika Ikulu ya Nairobi kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Alionyesha imani hiyo jana alipojiunga na wafanyakazi wa Ikulu katika ibada kwenye  ikulu hiyo ya Nairobi kwa ajili ya ibada ya madhehebu mbali mbali.

Katika hotuba yake fupi baada ya ibada, Rais Ruto alisema ana imani kwamba jengo jipya la maabadi litajengwa katika Ikulu hiyo ili kuchukua mahala pa jengo la sasa kwa nia ya kuhudumia waumini zaidi.

Kiongozi huyo wa nchi alisema kwamba kila Mkenya ana haki ya kumshukuru Mungu kwa baraka nyingi ambazo ametunukia taifa hili.

Haya yanajiri wiki mbili baada ya mahakama kuu kusimamisha mipango ya ujenzi wa kanisa hilo katika Ikulu kufuatia ombi lililowasilishwa na makundi manne ya uanaharakati.

Jaji Chacha Mwita aliitikia ombi la pamoja la shirika la Transparency International,Tume ya haki za binadamu nchini, shirika la Inuka Kenya ni Sisi na taasisi ya uwajibikaji katika jamii.

Wanaharakati hao walipinga mradi huo uliokusudiwa wa gharama ya shilingi bilioni 1.2 wakisema hata ingawa utafadhiliwa na raslimali za kibinafsi, unajengwa katika ardhi ya umma ilhali wakenya hawakuhusishwa.

Mahakama ilitenga Novemba 18, 2025 kuwa siku ya kikao cha kutathmini mawasilisho ya pande zote za kesi hiyo ambayo mahakama iliorodhesha kuwa ya dharura.

Share This Article