Rais William Ruto ameahidi kwamba ataendelea kushirikiana na viongozi wote nchini kwa ajili ya kuleta mabadiliko na ufanisi.
Kiongozi wa nchi alisema uwekezaji katika kilimo, Afya, Elimu na uundaji wa sera za kuhakikisha fursa za ajira ni muhimu badala ya kuangazia siasa zisizo muhimu.
Akihutubia viongozi wa eneo la Gusii katika Ikulu ya Nairobi leo, Rais Ruto alisema mabadiliko nchini Kenya yanaweza kuafikiwa iwapo viongozi watakuwa na msimamo sawia kuhusu maendeleo.
Katika mkutano huo, Rais alitaja miradi ya maendeleo katika magatuzi mawili ya eneo la Gusii itakayofaidi eneo hilo pakubwa ikiwa ni pamoja na nyumba elfu 15 za gharama nafuu kwa gharama ya shilingi bilioni 30, masoko manne makubwa ya gharama ya bilioni 2.4 na makazi ya wanafunzi ya bilioni 2.5 katika kaunti ya Kisii.
Nyamira Rais Ruto alisema serikali inaendesha miradi mikubwa huko ya thamani ya shilingi Bilioni 16, inayojumuisha nyumba elfu 7,000 , makazi ya wanafunzi na masoko.
Aliahidi kwamba makazi yapatayo elfu 32, katika kaunti za Kisii na Nyamira yataunganishwa na umeme na hivyo kufungua uchumi, kuwezesha viwanda na kuwapa wakazi vifaa vya kujiendeleza.
Mkutano huo ulihusisha viongozi waliochaguliwa katika kaunti za Kisii na Nyamira wakiongozwa na Gavana Paul Simba Arati na ulihudhuriwa pia na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.