Rais Erdogan: Netanyahu ni kizingiti cha amani Mashariki ya Kati

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemshutumu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, akimtaja kizingiti kikubwa cha amani ya kanda hiyo.

Erdogan alisema mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran kabla ya awamu mpya ya mazungumzo na Marekani kuhusu nyuklia, yalinuiwa kuhujumu mazungumzo hayo.

Akizungumza na wajumbe wa muungano wa mataifa ya kiarabu wakati wa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Mataifa ya Kiislamu Jijini Istanbul leo Jumamosi, Erdogan amezirai nchi zenye ushawishi kwa Israel kupuuza maamuzi yake na kutafuta suluhu kwa mapigano yanayoendelea kwa njia ya mazungumzo bila kuzidisha mzozo uliopo.

Erdogan alisema mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yanaonyesha kuwa Netanyahu na serikali yake hawataki mzozo huo utatuliwe kwa njia ya  kidiplomasia.

Erdogan alidai viongozi wa mataifa ya Magharibi yanatoa msaada kwa Israel bila masharti yoyote. Alisema serikali ya Uturuki haitaruhusu mipaka katika Mashariki ya Kati kurejeshwa katika mapigano.

Share This Article