Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amemwomboleza mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were aliyepigwa risasi na kufariki papo hapo Jumatano usiku, akimtaja kuwa kiongozi jasiri na aliyejitolea mhanga kwa kazi yake.
Were alipigwa risasi Jumatano jioni na watu waliokuwa kwenye pikipiki katika barabara ya Ngong, karibu na mzunguko wa City Mortuary.
Ripoti za polisi zinaarifu kuwa wauaji wa mbunge huyo, walikuwa wamepanga na kukusudia kumuua, huku Huduma ya Taifa ya Polisi ikianzisha uchunguzi kubaini chanzo cha mauaji hayo ya kinyama.
Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula amemataja mbunge huyo aliyekuwa akihudumu kwa muhula wa pili, kuwa kiongozi wa kupigiwa mfano.
Aidha, Wetang’ula alikashifu mauaji hayo akiwataka polisi kufanya uchunguzi wa haraka na kuwatia mbaroni wahusika.