Raila Odinga anatosha kuwa mwenyekiti wa AUC, asema Rais Ruto

Tom Mathinji
1 Min Read

Rais William Ruto, amezindua rasmi uwaniaji wa Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika AUC, huku akitoa wito wa umoja katika kanda ya Afrika Mashariki.

Akiwahutubiwa viongozi wa mataifa na wageni waliohudhuria hafla hiyo leo Jumanne katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto alisema  Kenya inaunga mkono azma ya Raila kuwa mwenyekiti wa muungano huo, kwani amewahi kuhudumu katika wadhfa wa mwakilishi wa miundo-mbinu barani humu.

“Tumekusanyika hapa kutangaza azma ya Raila Odinga kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Afrika AUC,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa Taifa alimtaja Raila kuwa kiongozi aliye na mageuzi na ambaye amejitolea kwa muda mrefu kupigia debe uongozi wa kidemokrasia na Umoja wa Afrika.

Alisema Raila ana tajriba ya uongozi unaohitajika na bara hili, ili liweze kupiga hatua.

“Odinga ni ni mwenye maono na aliye na rekodi njema ya kupigania mabadiliko na maendeleo barani humu,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto alisema kanda ya Afrika Mashariki iko tayari kuchukua hatamu za uongozi katika bara hili.

Aidha aliwahimiza viongozi wa Afrika, kumuunga mkono Odinga, akitaja hatua hiyo kuwa muhimu sana kwa Bara hili.

Share This Article