Raila Junior aahidi kuendelea kutunza familia yao

Marion Bosire
1 Min Read

Mwana wa kiume aliyesalia wa marehemu Raila Amolo Odinga, Raila Odinga Junior, ameahidi kwamba ataendelea kutunza familia yao, kufuatia kifo cha babake mzazi.

Junior alitoa ahadi hiyo wakati wa kusoma hotuba aliyoandaa ya kumwomboleza babake leo, wakati wa ibada ya wafu katika uwanja wa taifa wa Nyayo, akiwa amevaa kikofia alichopenda babake na kubeba mkia wa ng’ombe uliokaushwa.

Alisema anafahamu fika kwamba kakake mkubwa Fidel Castro hayuko kwani alishaaga dunia na sasa yeye ndiye mwanaume wa familia na atamtunza mamake Ida, na dada zake Winnie na Rosemary, pamoja na familia ya babake ya kisiasa.

Kando na familia, Raila Junior pia aliahidi kuendeleza masuala ambayo babake aliaminia sana kama kupigania uhuru, haki na usawa kwa wananchi wote.

Katika namna ya kipekee, Junior alihusisha waombolezaji waliokuwa wamekusanyika kwenye hotuba yake ambapo aliwaandalia kiitikio, “Asante Baba” kila aliposoma jambo ambalo marehemu babake alimfanyia.

Raila Amolo Odinga alifariki Oktoba 15, 2025 nchini India muda mfupi baada ya kufanya mazoezi yake ya asubuhi kama ilivyokuwa ada.

Share This Article