Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga amewasili katika kaunti ya Kisumu, siku moja baada ya kukutana na Rais William Ruto katika Ikulu ya Mombasa.
Raila alilakiwa na kaimu kiongozi wa chama cha ODM Prof. Anyang’ Nyong’o ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kisumu na viongozi wengine punde baada ya ndege yake kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu.
Kisha baadaye, Raila alishiriki mazungumzo na Prof. Nyong’o katika makazi ya Gavana huyo wa Kisumu.

Haijabainika ikiwa suala la uongozi wa chama wa ODM lilizugumziwa wakati wa mkutano baina yao.
Raila alimteua Prof. Nyong’o kuwa kaimu kiongozi wa chama hicho baada ya kuelezea azma ya kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Hata hivyo, azma ya Raila kutwaa uongozi wa AUC iligonga mwamba baada ya kushindwa na mpinzani wake mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf, aliyeteuliwa kuwa mrithi wa Moussa Faki Februari 15, 2025.
Raila amesema atatoa mwelekeo wake wa kisiasa baada ya kukutana na uongozi wa chama cha ODM, ingawa wengi wanatazamia kuwa atachukua tena uongozi wa chama hicho.
Aidha, haijabainika ikiwa atagombea tena urais ifikapo mwaka 2027 wakati kukiwa na uvumi kuwa huenda akamuunga mkono Rais William Ruto kutetea wadhifa wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Haijulikani ikiwa suala hilo lilijadiliwa wakati Ruto alipokutana na Raila katika Ikulu ya Mombasa jana Jumatatu.
Mizozo imetokota katika chama cha ODM kwa sasa huku baadhi ya wanachama wakionya dhidi ya chama hicho kuwa mfuasi sugu wa utawala wa sasa huku baadhi wakiunga mkono urafiki ibuka kati ya ODM na serikali ya Kenya Kwanza.