Raia mmoja wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 73, aliyepatikana na makosa mbalimbali ya kuwadhulumu watoto kimapenzi, amehukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani na kutozwa faini ya shilingi milioni tatu.
Jan Veld almaarufu Mwalimu Jan, Dad na Mzungu, pia imeagizwa alipe shilingi milioni tatu 3 zaidi, kama fidia kwa waathiriwa.
Masaibu ya Veld yalianza mwaka 2023, wakati video za kutatanisha zilizomwonyesha akioga na watoto wawili zilisambaa katika mitandao ya kijamii na kusababisha maafisa wa upelelezi kuanzisha uchunguzi mara moja.
Alipogundua anachunguzwa na maafisa wa polisi, mshukiwa huyo alijaribu kutoroka hapa nchini na kurejea Uholanzi lakini mipango yake haikufua dafu, kwani alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA.
Mahakama ya Milimani kuhusu watoto ilimpata Jan Veld, na hatia kwenye makosa sita ya uenezaji picha za ngono kwa watoto, makosa mawili ya mawasiliano ya kingono na mtoto, kosa moja la kutekeleza kitendo cha kingono na mtoto, na kosa moja la dhuluma dhidi ya watoto.
Mawakili wa upande wa mashtaka Linda Ndambiri na Victor Preston Owuo,r walisema kuwa mahakama hiyo iliarifiwa kwamba, Jan Veld alikuwa amemwonyesha mtoto wa umri wa miaka 17 aliyetambuliwa kuwa G.S picha na kanda za kingono kupitia mtandao wa WhatsApp, kwa lengo la kumhimiza mtoto huyo kujihusisha katika vitendo vya kingono.
Aidha mahakama iliamuru kwamba Jan Veld arejeshwe nchini mwao baada ya kukamilisha hukumu yake.