Idara ya polisi nchini Tanzania tawi la mkoa wa Mbeya, imetangaza kwamba inashikilia jamaa kwa jina Tadesa Limoli raia wa Ethiopia na wenzake 37.
Limoli wa umri wa miaka 32 na wenzake ambao wote ni wa kiume, walikamatwa kwa kosa la kuingia nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Katika taarifa, idara ya polisi ya Tanzania mkoa wa Mbeya ilielezea kwamba watuhumiwa walikamatwa mnamo Novemba 11, 2025 huko katika Pori la ranchi ya Matebete lililopo katika Kiji cha Igumbilo Shamba, Kata ya Chimala, Tarafa ya llongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya.
Walikuwa wanatumia usafiri wa gari yenye nambari za usajili T.953 DJF aina ya Toyota Noah mali ya Stanslaus Mazengo wa umri wa miaka 51, mkazi wa Isitu ambaye ndiye alikuwa akiendesha Gari hiyo.
Mazengo alielezea polisi kwamba alikuwa akiwapeleka kuwahifadhi wahamiaji hao haramu kwenye nyumba ya Jackline Malya wa umri wa miaka 26 mkazi wa Chimala.
Polisi katika taarifa yao walisema kwamba uchunguzi wao ulibaini watuhumiwa walikuwa wakiwasafirisha wahamiaji hao kwa njia ya kificho kwa lengo la kuwapeleka nchini Afrika Kusini.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linarai wananchi wenye tamaa ya fedha kuacha tabia ya kuwezesha raia wa kigeni kuingia au kupita nchini Tanzania bila kufuata taratibu za kisheria.
Badala yake wamehimizwa wawaelekeze kufuata taratibu kupitia mamlaka husika ili kuepuka usumbufu kama kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.