Ragga Dee apinga kuchaguliwa kwa wasanii zaidi kuwa viongozi

Maoni ya Ragga Dee yanajiri wakati ambapo Uganda inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Januari 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Ragga Dee ambaye jina lake halisi ni Daniel Kazibwe amepinga kuchaguliwa kwa wasanii zaidi kama wabunge nchini humo.

Akizungumza kwenye mahojiano, Dee aliangazia utendakazi wa wasanii waliochaguliwa wabunge katika bunge la sasa akionya dhidi ya kuongeza wazanii wengine uongozini katika ziku zijazo.

Msanii huyo anahisi kwamba kinachohitajika sio wasanii zaidi uongozini bali ni wabunge wanaojali watu wote, akiongeza kwamba mbunge mzuri ni yule ambaye anaweza kuzungumzia masuala mbali mbali yanayoathiri sekta tofauti.

“Mtazamo wangu ni kwamba ingawa wabunge wanapaswa kujali sekta wanazotoka, pia wanahitaji kufikiria kuhusu maeneo mapana wanayoyawakilisha,” alisema Dee.

Ragga Dee alipendekeza kuwa ongezeko la wasanii wanaoingilia siasa hivi karibuni lilichochewa zaidi na tamaa ya kupata faida ya kifedha.

“Hii ilikuwa kwa sababu wasanii waligundua kwamba pale ni mahali pa kupata pesa,” alieleza.

Wimbi hili limesababisha wasanii kadhaa maarufu kushinda nafasi za ubunge. Miongoni mwa wasanii waliopata ushindi katika Bunge la 11 ni Geoffrey Lutaaya, mwanamuziki maarufu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kakuuto, Hilary Innocent Kiyaga anayefahamika kama Dr. Hilderman na Racheal Magoola wa Bendi ya Afrigo.

Hata hivyo, Ragga Dee alidai kuwa siasa ni mchezo tofauti kabisa, unaohitaji ujuzi maalum ambao wasanii wengi hao hawajaweza kuonyesha.

Kwa mujibu wa Ragga Dee, siasa inahitaji maandalizi ya kina na uelewa wa hali halisi ya matatizo yanayowakumba wananchi.

Alibainisha kuwa mbunge makini anapaswa kuwa msomaji mzuri, aelewe takwimu na aweze kuelezea matatizo ya wapiga kura wake kwa ufasaha.

Maoni yake ni kwamba wasanii wengi walioko bungeni kwa sasa hawajakidhi matarajio haya.

Share This Article