Radi wakati wa vimbunga vya monsuni mashariki mwa India wiki hii zimewaua watu wasiopungua 33 na kujeruhi makumi ya wengine nchini humo.
Hayo yamesemwa na maafisa nchini humo leo Ijumaa.
Vifo katika jimbo la Bihar vilitokea wakati wa vimbunga vikali kati ya juzi Jumatano na jana Alhamisi.
Idara ya usimamizi wa majanga ya jimbo hilo imesema waathiriwa walikuwa hasa wakulima na wafanyakazi waliofanya kazi katika maeneo ya wazi.
Mvua kubwa zaidi na radi zinatabiriwa kutokea katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo.
Waziri wa Usimamizi wa Majanga katika jimbo la Bihar, Vijay Kumar Mandal, aliiambia AFP kuwa maafisa katika maeneo hatari wameagizwa “kukuza hamasa ili kuchukua hatua za tahadhari kufuatia tangazo juu ya radi”.
Serikali ya jimbo hilo imetangaza fidia ya rupia milioni 4 ambazo ni sawa na dola 4,600 kwa familia za wale waliouawa na radi.
Watu wasiopungua 243 walifariki baada ya kupigwa na radi mnamo mwaka 2024 na watu 275 mwaka uliotangulia, kwa mujibu wa serikali ya jimbo hilo.
Eneo la mashariki mwa India, ikiwemo Bihar, hukumbwa na mafuriko kila mwaka ambayo huua makumi ya watu na kufanya mamia ya maelfu ya wengine kupoteza makazi wakati wa kilele cha msimu wa monsuni.