Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Tanzania wa mtindo wa Hip Hop Profesa Jay amewatetea wanamuziki ambao wanalaumiwa na wengi kwa kuhusika kwenye kampeni za vyama mbali mbali vya kisiasa.
Ikumbukwe kwamba uchaguzi mkuu utaandaliwa nchini humo mwezi Oktoba mwaka huu na hiki ni kipindi cha kampeni.
Kwa kawaida wanasiasa na vyama vya kisiasa hutumia mbinu mbali mbali kuvutia wapiga kura kama vile kuhusisha wanamuziki kwenye mikutano ya kampeni kutokana na ushawishi wao.
Sasa Jay ambaye alikuwa akizungumza kwenye mahojiano na Millard Ayo anasema sio vizuri kudhalilisha wanamuziki kwa sababu hiyo kwani Tanzania ni nchi ya kidemokrasia.
Aliendelea kusema kwamba wasanii binafsi wana upande wanaopendelea kisiasa na wanaruhusiwa kufanya hivyo kwani ni haki yao ya kimsingi.
Kulingana naye, miegemeo ya kisiasa haifai kuathiri undugu na alitoa mfano wake mwenyewe kwani yeye ni wa chama cha CHADEMA lakini alipougua usaidizi ulitoka pande zote hata chama tawala cha CCM.
Suala hili liliibuka kufuatia jinsi mwanamuziki AY alishambuliwa na wengi kwa kuonekana mara ya kwanza akichagua kuunga mkono chama tawala cha CCM kwenye kampeni zinazoendelea.
Huku hayo yakijiri, Jay kupitia kwa wakfu wake almaarufu Profesa Jay Foundation anapanga tukio la kuelimisha watu kuhusu maradhi ya figo.
Shughuli hiyo itafanyika Ijumaa Machi 14, 2025 katika ukumbi wa Ummy Mwalimu ulioko katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam.
Profesa Jay aliugua maradhi ya figo kwa muda mrefu na afueni yake hutizamiwa na wengi kuwa muujiza. Baada ya kuondoka hospitalini, alibuni wakfu ambao huwa anatumia kuchangisha pesa za kusaidia wasiojiweza kugharamia matibabi ya figo na pia kutoa uhamasisho kuhusu maradhi hayo.