Prof. Kindiki kuapishwa kama Naibu Rais

Martin Mwanje
1 Min Read

Prof. Kithure Kindiki yuko huru kula kiapo cha kuhudumu kama Naibu Rais.

Hii ni baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ambao ni Eric Ogola, Anthony Mrima na Dkt. Freda Mugambi kuondoa maagizo yaliyozuia kuapishwa kwake kama Naibu Rais.

Prof. Kindiki aliteuliwa na Rais William Ruto kuwa Naibu Rais baada ya Bunge la Seneti kudhinisha mashtaka 5 kati ya 11 yaliyokuwa kwenye hoja ya kumbandua Rigathi Gachagua.

Hata hivyo, baada ya kupigwa teke na Seneti, Gachagua alipata maagizo ya mahakama kuzuia kuapishwa kwa mrithi wake akidai mchakato wa kumbandua madarakani haukuwa wa haki.

Mwanasheria Mkuu, Bunge la Taifa na lile Seneti waliwasilisha kesi mahakamani wakitaka maagizo hayo yaondolewe ili kupisha kuapishwa kwa Prof. Kindiki.

Katika kuwasilisha kesi hiyo, pande hizo zote zilisema Gachagua alikoma kuwa Naibu Rais punde baada ya kubanduliwa kwake kuidhinishwa na Bunge la Seneti kwa mujibu wa kifungu cha 145(7).

Ombi ambalo mahakama imeridhia kwa kuondoa maagizo hayo wakati kesi ya Gachagua ikiendelea kusikilizwa.

Mawakili wa Gachagua wameashiria kuwa watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Share This Article