Prince Indah na Chameleone washirikiana

Prince Indah ametangaza ujio wa kibao chao cha pamoja Juni 9, 2025.

Marion Bosire
1 Min Read

Wanamuziki Prince Indah wa Kenya na mkongwe wa muziki nchini Uganda Jose Chameleone wameshirikiana kikazi katika kazi iitwayo ‘The Way You Are’.

Haya yalibainika kutokana na chapisho la Prince Indah mitandaoni lenye bango la kibao hicho kilichoandaliwa na kampuni ya Easy Music Africa na ile ya Malaika.

“Kazi iliyosubiriwa kwa muda ndiyo hii hapa. Kenya yakutana na Uganda! ‘The Way You Are'” aliandika Prince Inda akiendelea kuelezea kwamba ameshirikiana na bingwa huyo wa muziki nchini Uganda kuletea mashabiki wake wimbo wa kipekee.

Kulingana naye kazi hiyo ya sanaa inayotarajiwa kuzinduliwa rasmi Juni 9, 2025, inasherehekea moyo, utamaduni na mdundo wa Afrika Mashariki.

“Historia itaandikishwa. Muziki utazungumza. Mipaka haitaonekana. Huu ni zaidi ya wimbo ni vuguvugu” aliendelea kusema Indah katika chapisho lake huku akiwatia mashabiki zake hamu kwa kudai kwamba ushirikiano wake na Chameleone utatikisa eneo hili na kuhamasisha ulimwengu.

Chameleone amewahi kushirikiana na wanamuziki wengine wa Kenya akiwemo Redsan na JuaCali, lakini kazi hii huenda ikawa na mashiko zaidi kutokana na umaarufu ambao Prince Indah amejizolea nchini.

Share This Article