Msanii wa muziki nchini Nigeria, Habeeb Okikiola, maarufu kama Portable, kwa mara nyingine amesema anataka kupambana na bingwa wa zamani wa uzani wa juu mara mbili, Anthony Joshua, ambaye kwa sasa yuko likizo nchini Nigeria, katika ulingo wa ndondi.
Haya yanajiri baada ya Portable kushinda kwenye pambano la ndondi la nyota wa muziki dhidi ya Darlington Okoye maarufu kama Speed Darlington, lililofanyika Jumamosi.
Mwimbaji huyo wa wimbo wa “Zazu” alitawala pambano hilo kwa kiasi kikubwa, akimsababishia maumivu makubwa Speed Darlington hadi akashindwa kurejea kwa raundi ya pili, hatua iliyompa Portable ushindi kwa Technical Knockout (TKO).
Msanii huyo mwenye utata alishinda katika pambano la ndondi la mastaa lililopatiwa jina la “Chaos In The Ring” lililofanyika katika Ukumbi wa Balmoral jijini Lagos, Jumamosi Aprili 19, 2025.
Wasiwasi ulishuhudiwa hata kabla hata ya pambano lenyewe, wakati wasanii hao walizozana wakati wa kupima uzani hali iliyolazimu waandaaji kuingilia kati na kuwatenganisha.
Mara tu kengele ya raundi ya kwanza ilipopigwa, Portable hakupoteza muda kuonyesha ubabe wake.
Alimrushia Darlington makonde ya haraka-haraka, akionyesha hatua za miguu za wepesi na mashambulizi yasiyokwisha. Rais huyo wa Zee Nation alimfinya mpinzani wake mara kwa mara, akiendelea kumzamba makonde hadi mwisho wa raundi.
Mashabiki walifurahia kuona uhasama wa muda mrefu wa mitandaoni kati ya mastaa hao wawili wenye utata ukitafsiriwa katika ulingo wa ndondi.
Hata hivyo, pambano hilo lilimalizika ghafla baada ya Speed Darlington, aliyekuwa na bandeji kwenye mkono wa kulia, kukataa kuendelea na raundi ya pili, hivyo kumpa Portable ushindi kwa Technical Knockout.
Baada ya pambano, Speed Darlington alimtuhumu Portable kwa kutumia nguvu za kishirikina wakati wa pambano hilo.
Wakili wake kwa jina Deji Adeyanju, anataka pambano lirudiwe, akidai uamuzi mbaya kutoka kwa waamuzi na kutaka raundi ya pili yenye haki kupitia taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook.