Portable amrushia VDM maneno baada ya kumtaja

VDM alisema anataka kumhusisha Portable kwenye wimbo wa kumtukana Mercy Chinwo.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Nigeria Portable amemjibu mwanamitandao na mkosoaji Very Dark Man – VDM baada ya VDM kumtaja akisema angetaka kumhusisha kwenye wimbo.

Wimbo huo kulingana na VDM ni wa kumtusi mwimbaji wa nyimbo za injili Mercy Chinwo. Chinwo amewasilisha kesi mahakamani dhidi ya VDM kufuatia maneno aliyoyasema kuhusu mgogoro wa Chinwo na meneja wake wa zamani.

Portable alirekodi video ya kumjibu VDM akisema, “VDM au jina lolote wanalokuita. Koma kunizungumzia. Unajua watu hunilipa pesa ngapi kunihusisha kwenye nyimbo zao?”

Aliendelea kwa kumuuliza iwapo anaweza kumudu Naira milioni 100, ishara kwamba hicho ndicho kiasi cha pesa ambacho yeye hulipisha wanaotaka kushirikiana naye.

Wiki kadhaa zilizopita, Mercy Chinwo alichapisha video ya kuzungumzia ugomvi unaojiri kati yake na aliyekuwa meneja wake Ezekiel Thankgod Onyedikachukwu maarufu kama EeZee Tee.

Katika video hiyo alielezea masaibu mbali mbali aliyopitia mikononi mwa EeZee Tee kiasi cha kububujikwa na machozi.

VDM alitoa maoni yake kuhusu madai ya Chinwo akimlaumu kwa kile alichokitaja kuwa kutokuwa mkweli na kubana mambo kadhaa kwenye kesi kati yake na EeZee Tee.

Chinwo alikasirishwa na usemi wa VDM na akachukua hatua ya kuwasilisha kesi dhidi yake mahakamani akimlaumu kwa kumchafulia jina na anadai fidia.

Awali, VDM alikuwa ameamua kuchukua mkondo wa kuomba msamaha kutoka kwa Chinwo akisema kwamba hawezi kumudu kumlipa fidia iwapo atamshinda kwenye kesi hiyo.

Sasa anaonekana kuamua kuendeleza uchokozi dhidi ya Chinwo.

Share This Article