Polisi watatu wa trafiki wakamatwa kwa kupokea mlungula

Tom Mathinji
1 Min Read
Maafisa watatu wa polisi wa trafiki wakamatwa kwa kupokea mlungula.

Maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC),  wamewakamata maafisa watatu wa polisi wa trafiki, waliokuwa wakipokea hongo kutoka kwa wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma kwenye mzunguko wa Globe Cinema jijini Nairobi.

EACC kupitia ukurasa wake wa X, ilisema ilitekeleza operesheni hiyo baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa umma, kuhusu maafisa hao wa trafiki waliokuwa wakiwaitisha hongo kwa kisingizio wamekiuka sheria za trafiki.

“Mnamo Jumatano Februari 12, 2025, EACC ilitekeleza operesheni katika mzunguko wa Globe na kuwakamata maafisa watatu wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Central ambao walikuwa wamekusanya hongo ya shilingi 48,250 kwa muda wa saa mbili kuanzia saa kumi na mbili jioni,” ilisema EACC.

Maafisa hao waliokamatwa ni pamoja na Oscar Serem Biwott wa nambari 84220, Simon Kiplagat wa nambari 89197 na Edwin Benedict wa nambari ya kazi 82069.

Baadaye, walipelekwa hadi katika makao makuu ya EACC walikoandikisha taarifa, kabla ya kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani wakisubiri kuchukuliwa hatua zaidi.

TAGGED:
Share This Article