Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamemuokoa mtoto wa umri wa miaka mitatu, aliyekuwa ameibwa kutoka nyumbani kwao Ruiru, kaunti ya Kiambu, ambapo washukiwa wawili walikamatwa.
Baada ya wazazi wa mtoto huyo kuripoti katika kituo cha polisi cha Ruiru, maafisa hao walianzisha uchunguzi mara moja, uliowapeleka Magharibi na Kati kati mwa nchi washukiwa hao walikofumaniwa.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema kuwa mshukiwa mmoja alikamatwa katika nyumba moja eneo la Tetu kaunti ya Nyeri, ambapo polisi walimpata mtoto huyo akiwa na mmiliki wa nyumba hiyo George Maina, pamoja na mwanamume anayedaiwa kumuiba mtoto huyo
Kulingana na DCI, licha ya kuwa wazazi wa mtoto huyo wamefahamshwa kuhusu kuokolewa kwake, mtoto huyo kwa sasa anafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu hospitalini,kabla ya kuunganishwa nao.
Kutiwa nguvuni kwa washukiwa hao kunajiri wakati ambapo visa vya watoto kupotea vimeongezeka kote nchini, swala ambalo limezidisha wasiwasi katika kitengo cha kukabiliana na ulanguzi wa watu na ulinzi wa watoto.