Mbunge wa Naivasha Jane Kihara amekamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kwa madai ya kukaidi agizo la kufika mbele ya idara hiyo kuhusiana na madai ya uchochezi na kudharau mamlaka ya afisa wa umma.
Kihara alisafirishwa kutoka nyumbani mwake katika mtaa wa Maraigushu hadi kituo cha polisi cha Naivasha, ambapo alikanusha madai ya kuhusika na ghasia zilizoshuhudiwa mjini Naivasha ambapo wafanyabiashara kadha walipoteza mali yao.
Akizungumza katika kituo cha polisi cha Naivasha, Kihara alisema kumatwa kwake chini ya kifungu cha 132 ni kinyume cha sheria.
“Mawakili wangu waliiandikia idara ya DCI kuifahamisha kwamba agizo lililotolewa ni kinyume cha sheria, lakini wameamua kunikamata,” alisema Mbunge huyo.
Aidha alidai kukamatwa kwake ni njama ya kumhujumu.huku akijitenga na ghasia hizo.
“Hii ni njama ya kuwakandamiza wale wanaopinga utawala wa sasa,” alidokeza mbunge huyo.