Huduma ya Taifa ya Polisi , NPS, imekanusha kuhusika na mauaji ya Juliet Wangai Kariuki wakati wa maandamano ya Saba Saba tarehe saba mwezi huu mjini Nanyuki.
Kulingana na taarifa ya NPS, marehemu Kariuki alikuwa miongoni mwa waandamanaji 126 waliokamatwa na polisi katika maandamano hayo na kufikishwa katika mahakama ya Nanyuki Julai 8.
Wote walikanusha kuwa na hatia kwa makosa ya kuharibu mali kwa kukusudia na uporaji, na kuamriwa walipe dhamana ya shilingi 50,000 kila mmoja.
Marehemu Kariuki alipatikana amefariki akiwa gerezani, hali ambayo imeibua mvutano kati ya Idara ya Magereza na NPS kuhusu nani aliyesababisha kifo cha mwandamanaji huyo.
NPS imeongeza kuwa hakuna malalamishi yoyote yaliyowasilishwa dhidi yake hadi leo kuhusiana na kifo hicho.
Hata hivyo, polisi wameapa kufanya uchunguzi wa mauaji hayo na wote waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria.