Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Malindi, kaunti ya Kilifi wamefanya operesheni kali iliyoyalenga magenge ya wahalifu katika eneo la Soweto katika kaunti ndogo ya Malindi.
Hii ni baada ya kupokea taarifa za kijasusi kuhusiana na shughuli za magenge hayo.
Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS inasema wakati wa operesheni hiyo, washukiwa 7 walikamatwa wakiwa na silaha butu.
Washukiwa hao kwa sasa wamezuiliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani.
NPS inatoa wito kwa umma kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia kuyaangamiza magenge hayo kupitia nambari zisizotozwa malipo ambazo ni 999, 911, 112 au nambari ya WhatsApp 0709 570 000.