Polisi wagundua kiwanda haramu cha Pombe kaunti ya Kiambu

Shughuli za kutengeneza na kupakia pombe zilikuwa zikiendelea katika ghorofa ya chini ya nyumba ya kifahari yenye orofa mbili mtaani Kahawa Sukari.

Marion Bosire
3 Min Read

Maafisa wa polisi katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, walivamia kiwanda haramu cha kutengeneza pombe katika makazi ya kifahari mtaani Kahawa Sukari na kukapata lita 1,000 za kemikali ya ethanol na aina mbalimbali za pombe bandia za thamani isiyojulikana.

Kikosi cha pamoja kilichojumuisha maafisa wa mamlaka ya kukusanya ushuru -KRA, polisi wa utawala na polisi wa kawaida kiliweka mtego na kukamata washukiwa wawili waliokuwa wakifanya kazi katika jengo hilo kwenye barabara ya Isiolo 2nd South Avenue.

Kamanda wa polisi wa eneo hilo, Charles Kibathi, aliambia wanahabari kwamba mshukiwa mkuu aliyekuwa amekomboa nyumba hiyo kutoka kwa mjane fulani alifanikiwa kukwepa mtego wa polisi, lakini maafisa bado wanamfuatilia kwa kutumia taarifa za siri.

Maafisa kwa ushirikiano na viongozi wa chama cha wakazi wa mtaa huo walifanya msako katika makazi hayo ambapo waligundua shughuli za kutengeneza na kupakia pombe zikiendelea katika ghorofa ya chini ya nyumba hiyo ya kifahari yenye orofa mbili.

Mmiliki wa nyumba hiyo aliikodisha na kuhamia kijijini.

Kibathi alisema takribani chupa 10,000, katoni 126, stempu za KRA, vifaa vya kutengenezea pombe, matenki ya maji na vizibo vya chupa vilipatikana katika eneo hilo na ushahidi wote ulipelekwa katika maghala ya KRA jijini Nairobi kwa hifadhi salama huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Viongozi wa wakazi wakiongozwa na mwenyekiti wa chama cha wakazi wa Kahawa Sukari, Samuel Mwaniki, walifichua kwamba mtu anayeendesha biashara hiyo haramu alikodisha jengo hilo mwezi Desemba mwaka jana.

Mwaniki alisema sio mara ya kwanza kwa kiwanda cha kutengeneza pombe kupatikana katika mtaa huo na kuwataka wakazi kushirikiana na maafisa wa usalama kutokomeza wanaotengeneza na kuuza pombe haramu kwa wateja wasiojua, hasa vijana.

Mwakilishi wa Wadi wa eneo hilo, Kennedy Odhiambo, alisema biashara hiyo haijasajiliwa na serikali ya kaunti na kuwataka wenyeji kuwa waangalifu dhidi ya matapeli wanaodai kuendesha biashara halali.

Pia aliwataka wamiliki wa nyumba kuhakikisha mikataba ya upangaji na taarifa za wapangaji zinashirikiwa na maafisa wa utawala na usalama.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Ruiru, Julius Too, alisema serikali haitakubali biashara kama hizo kuendelea katika maeneo ya makazi na alieleza kuwa mshukiwa mkuu anaonekana kuendesha biashara kama hiyo katika maeneo mengine.

Share This Article