Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha Mwalimu Mkuu wa shule ya upili ya wavulana ya Kaplong, Mike Yator.
Yator alifariki Jumanne asubuhi akiwa katika nyumba yake iliyo shuleni huku kifo chake kikiwashangaza wengi.
Kamishna wa polisi wa kaunti ya Bomet Edward Ibwaga, ametoa hakikisho la kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kifo cha Yator.
Chama cha walimu wa shule za sekondari na vyuo, KUPPET, kimewataka polisi kufanya uchunguzi, kwani marehemu Yator hakuwa na dalili zozote za ugonjwa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya shule hiyo, Edmond Rono, ambaye alikuwa shuleni akifanya kazi hadi Jumatatu wiki hii, naye alisema marehemu hakuonyesha dalili za ugonjwa.
Yator alionekana akiwakaribisha wanafunzi shule Jumatatu wiki hii walipokuwa wanarejea kutoka likizo fupi ya katikati ya muhula.
Mwili wa marehemu ulipatakana kwenye sakafu ya chumba chake mapema Jumanne.