Maafisa wa polisi wa kupambana dhidi ya mihadarati (ANU) mjini Malindi, na kikosi maalum cha polisi (SOG) katika daraja la Sabaki, walifumania gari aina ya Toyota SUV lililokuwa likisafirisha magunia 12 ya bangi.
Polisi hao waliokuwa wamepokea vidokezo walisimamisha gari hilo lenye nambari za usajili KCK 810C, katika kituo cha ukaguzi cha Gede, ila dereva akakaidi ndiposa wakaanza kulifuata.
Gari hilo baadaye lilipatikana limeachwa katika eneo la Mayungu huku nambari za usajili zikiwa zimebadilishwa hadi KCJ 752Z.
Gari hilo pamoja na bangi ya thamani ya mamilioni ya pesa zilipelekwa katika kituo cha polisi cha Malindi huku dereva wake akisakwa.