Serikali ya Uganda imezindua mpango makhsusi wa kujaribu kukabiliana na ufisadi kati ya maafisa wa polisi kwa kuleta kamera za kuvaa mwilini wakiwa kazini.
Mpango huo ambao umeelezewa kwa kina kwenye manifesto ya chama tawala NRM iliyozinduliwajana Jumatatu September 29 na Rais Yoweri Museveni katika hoteli ya Speke huko Munyonyo.
Unatarajiwa kuboresha ufuatiliaji, kuimarisha uwajibikaji na kupunguza vitendo vilivyo kinyume cha sheria katika sekta ya utekelezaji sheria, ambayo imepoteza imani ya umma kwa kiwango kikubwa.
Shinikizo za kuwepo kwa kamera hizo zinalenga idara ambayo wananchi wengi wa Uganda wanachukulia kuwa yenye kiwango kikubwa cha ufisadi.
Ripoti kadhaa ikiwemo ya uchunguzi kuhusu uadilifu wa taifa, zimekuwa zikiweka polisi wa Uganda kati ya idara mbovu kabisa kwa kuchukua hongo kutoka kwa wananchi.
Kiwango cha utozaji hongo kiko juu katika idara ya polisi wa trafiki na ile ya upelelezi wa jinai.
Mataifa mbali mbali ulimwenguni yanatekeleza hatua hiyo ya polisi kuwa na kamera za kuvaliwa mwilini na huwa zinanasa matukio yote katika utendakazi wa maafisa hao wa polisi.
Lengo kuu la vifaa hivyo ni kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na kukusanya ushahidi.Nchi ambazo polisi wake wanatumia vifaa hivyo ni pamoja na Uingereza, Japan na Marekani.