Polisi wa Kenya aliyetoweka wakati wa operesheni nchini Haiti amethibitishwa kufariki.
Idara ya Taifa ya Polisi (NPS) imethibitisha kifo cha polisi huyo aliyekuwa sehemu ya Kikosi cha Kimataifa cha Kudumisha Usalama nchini Haiti (MSSM).
“Afisa huyo aliripotiwa kutoweka wakati akiwa kazini Machi 25, 2025 kufuatia uvamizi uliofanywa kwenye njia kuu ya usambazaji ya Carrefour Paye-Saven katika eneo la Pont-Sonde la Idara ya Artibonite,” ilisema NPS kupitia msemaji wake Muchiri Nyaga kwenye taarifa.
Nyaga akisema waliitarifu familia ya marehemu punde baada ya kuthibitishwa kwa kifo cha afisa huyo.
NPS imetuma risala za rambirambi kwa familia ya afisa huyo kutokana na kifo chake.
Aidha, idara hiyo inasema inafanya kazi kwa karibu na Polisi wa Taifa wa Haiti (HNP) kuhusiana na suala hilo na kwamba itatoa maelezo zaidi punde baada ya kupata taarifa.
Wakati huohuo, mwili wa Koplo Kennedy Mutuku Nzuve aliyefariki kwenye ajali ya barabarani umepangiwa kurejeshwa humu nchini kesho Ijumaa, Septemba 26.
Nzuve alifariki kwenye ajali hiyo iliyotokea Septemba 1, 2025.