Police FC wametanua uongozi wa pointi tatu kileleni pa jedwali la ligi kuu ya Kenya FKFPL baada ya kusajili ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bidco United, katika mechi ya Jumamosi jioni uwanjani Kenyatta kaunti ya Machakos.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizikia sare tasa, Mohammed Bajaber aliwaweka kifua mbele maafande kwa goli la dakika ya 69, kabla ya nguvu mpya David Simiyu kutikisa nyavu kwa bao la pili dakika ya 72.
Police FC wanaongoza jedwali kwa pointi 41, wakifuatwa na Tusker FC kwa alama 38, huku mabingwa watetezi Gor Mahia, wakikalia nafasi ya tatu kwa pointi 34.
Katika matokeo mengine Sofapaka waliimenya KCB 2-0, AFC Leopards ikaikwatua Mara Sugar 2-1, huku Talanta FC ikielea baharini baada ya kuwazima Bandari FC 3-2.
Muranga Seal walipigwa nyumbani magoli 2-1 na wanajeshi Ulinzi Stars.