Philip Karanja mwandaaji na mwelekezi wa filamu nchini Kenya amelazwa hospitalini baada ya kujeruhiwa mguu.
Rafiki yake wa karibu ambaye pia anajihusisha na maandalizi ya filamu na uigizaji Abel Mutua ndiye alitangaza hayo kupitia mitandao ya kijamii.
Mutua alichapisha video fupi inayomwonyesha Philip akitembea huku akitumia fremu ya kutembea na kuchechemea hospitalini na kuelezea kwamba alijaribu kucheza mpira akavunjika mguu.
Abel alifichua pia kwamba ilibidi Philip ambaye anafahamika pia kama Phil Director afanyiwe upasuaji na awekewe chuma mguuni.
Phil Director naye alichapisha picha zinazomwonyesha akiwa hospitalini na kuandika maneno ya utani kwamba amenguka na anatumia mguu mmoja akiashiria wimbo unaosambaa kwa kasi wa Gen Z “Anguka Nayo”.
Huku wengi wakimtakia afueni ya haraka mitandaoni, marafiki wake waliamua kumtania. Mwigizaji na mchekeshaji Njugush alimtakia kila la kheri anapokwenda ‘kijufungua’ utani uliolenga vazi la hospitali alilokuwa amevalia.
Mchekeshaji mwingine kwa jina Njoro alimtakia afueni ya haraka na kuongeza “Hii ndio ile miaka mtu huacha kula vitu vilivyo na sukari.”
Mwigizaji Cate Actress ambaye alikuwa mke wa Phil alimtaka aongeze hifadhi yake ya virutubisho vya mwili aina ya Calcium huku Tash Kay akiandika, “Haujapona moyo tangu uvunjwe na sasa unataka kuvunjika miguu?”.
Tunamtakia Phil Director afueni ya haraka.