Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis aliyefariki Jumatatu, atazikwa siku ya Jumamosi saa nne asubuhi, hayo ni kulingana na makao makuu ya kanisa Katoliki Vatican.
Kulingana na Vatican, mwili wa Papa Francis utasafirishwa kutoka kanisa la Casa Santa Marta, hadi katika kanisa la St. Peter’s Basilica siku ya Jumatano saa tatu asubuhi, na utasalia hapo hadi siku ya mazishi.
Mazishi hayo ya Papa Francis yataongozwa na Kadinali Giovanni Battista Re, ambaye ni mkuu wa taasisi ya makadinali. Mazishi hayo yatahudhuriwa na Makadilali, makasisi, Ma-Askofu na Ma-Askofu wakuu kutoka pembe zote za dunia.
Katika ukurasa wa X, Vatican ilitoa picha za Papa Francis katika jeneza lililo wazi, akiwa amevalia vazi jekundu na kilemba cha papa kichwani na rozari mkononi.
Kifo cha papa kimeibua huzuni nyingi miongoni mwa waumini wa kanisa la katoliki kote ulimwenguni.