Papa Francis amefariki

Ripoti kutoka makao makuu ya kanisa katoliki ulimwenguni zinaashiria kwamba Papa Francis ameaga dunia leo asubuhi.

Marion Bosire
2 Min Read
Papa Francis.

Kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis amefariki akiwa na umri wa miaka 88.

Kulingana na taarifa ya Kadinali Kevin Ferrell ambaye ni msimamizi mkuu wa Vatican, Papa Francis ameaga dunia leo, Aprili 21, 2025 katika makazi yake ya Casa Santa Marta ndani ya Vatican saa moja na dakika 35 asubuhi.

“Saa moja na dakika 35 asubuhi ya leo, Askofu wa Roma, Francis, alirejea nyumbani kwa baba.” alisema Kadinali Ferrell akiongeza kusema kwamba Papa Francis alikuwa ametoa maisha yake yote kwa huduma kwa Mungu na kwa Kanisa.

Ferrell aliendelea kusema kwamba Francis aliwafundisha waishie maadili ya injili kwa uaminifu, ujasiri na upendo kwa wote hasa kwa maskini na waliotengwa katika jamii.

Papa Francis ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, alizaliwa katika eneo la  Flores,  jijini  Buenos Aires, nchini  Argentina Disemba 17, 1936 na alikuwa kifungua mimba wa wazazi wake Mario José Bergoglio na Regina María Sívori.

Amekuwa kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni tangu Machi 13, 2013 na ndiye wa kwanza kutoka kwa shirika la mapadri la Jesuit kuwahi kuongoza Kanisa hilo ulimwengu mzima.

Februari 14, 2025 Papa Francis aliripotiwa kuugua na kulazwa katika hospitali ya Gemelli jijini Roma kutokana na maradhi ya homa ya mapafu.

Jumapili Machi 23, 2025 Papa aliruhusiwa kuondoka kwenye hospitali hiyo ili aendelee kupata nafuu katika makazi yake.

Jana Jumapili takatifu ya msimu wa Pasaka, kiongozi huyo aliweza kujumuika na waumini kwa ibada katika uwanja wa St. Peters’ Square.

Share This Article