Alice na Ellen Kessler ambao ni pacha wazaliwa wa Ujerumani waliokuwa maarufu miaka ya 1950 hadi 1960 kwa kucheza densi, kuimba na hata kuigiza wamefariki.
Inaripotiwa kwamba waliamua kufa pamoja kwa kujitoa uhai.
Kulingana na vyombo vya habari nchini Ujerumani, wawili hao walifariki nyumbani kwao karibu na Munich, Ujerumani, kupitia kusaidiwa kujitoa uhai.
Kulingana na ripoti, wawili hao hawakutaka kuendelea kuishi na walikuwa wamechagua kumaliza maisha yao pamoja na mamlaka ziliripotiwa kufahamishwa baada ya vifo vyao.
Nchini Ujerumani, msaada wa kujitoa uhai unaruhusiwa katika hali fulani, kufuatia uamuzi wa mwaka 2020 wa mahakama ya juu ya nchi hiyo, uliobaini kuwa watu wana haki ya kumaliza maisha yao kupitia usaidizi wa mtu mwingine — mradi tu uamuzi huo unafanywa kwa hiari na bila shinikizo la nje.
Mwaka jana, pacha hao wa Kessler waliiambia jarida la Bild kuwa walitaka majivu yao yawekwe kwenye chungu kimoja na kuzikwa karibu na mama yao na mbwa wao.
Dada hao walipata umaarufu kutokana na uimbaji na uchezaji densi, na katika kazi yao ndefu na yenye mafanikio, walishiriki majukwaa na wakongwe kama Frank Sinatra, Fred Astaire na Dean Martin.
Wakitunukiwa jina “Miguu ya Taifa” na walikuwa maarufu kwenye vipindi vya runinga vya Italia na pia walionekana kwenye vipindi maarufu vya Marekani kama “The Ed Sullivan Show” na “The Dean Martin Show.”
Alice na Ellen walikuwa na umri wa miaka 89.