P. Diddy apatikana bila hatia kwenye makosa matatu makuu

Mwanamuziki huyo sasa anakabiliwa na kifungo cha jumla ya miaka 20 gerezani kutokana na makosa mawili.

Marion Bosire
2 Min Read
P Diddy

Mwanamuziki wa Marekani P. Diddy alipatikana kuwa hana hatia kwenye makosa matatu kati ya makosa matano yaliyokuwa yakimkabili katika kesi dhidi yake.

Baada ya majadiliano ya jumla ya saa 13, jopo la waamuzi liliafikia kwamba Diddy hana hatia katika kosa la kwanza la uhalifu wa kupanga ambalo adhabu yake kubwa zaidi ingekuwa kifungo cha maisha gerezani.

Katika kosa la pili linalohusu ulanguzi wa binadamu kwa matumizi ya kingono, ambalo lilitokana na malalamishi ya aliyekuwa mpenzi wake Cassie Ventura, Diddy alipatikana bila hatia.

Kosa hilo lingevutia adhabu ya kifungo cha miaka 15 hadi maisha gerezani.

Kosa la tatu lilihusu usafirishaji wa binadamu na kumlazimisha kushiriki ukahaba na lilitokana pia na malalamishi ya Cassie. Diddy ana hatia katika kosa hilo na adhabu yake ya juu zaidi ni kifungo cha miaka 10 gerezani.

Kosa la nne lilihusu ulanguzi wa binadamu kwa ajili ya kumtumia kingono, kumlazimisha kutenda mambo asiyoyataka na ulaghai. Lilitokana na malalamishi ya mwathiriwa wa pili ambaye utambuzi wake ulifichwa na mahakama.

Diddy hakupatikana na hatia kwenye kosa hilo la nne ambalo lingevutia adhabu ya kifungo cha miaka 15 hadi maisha gerezani.

Mwanamuziki huyo alipatikana na hatia kwenye kosa la tano na la mwisho kwenye kesi yake lile la kusafirisha mtu kwa nia ya kumshirikisha katika ukahaba kutokana na malalamishi ya mwathiriwa huyo wa pili wa kike ambaye hakutana utambuzi wake uwekwe wazi.

Uamuzi huo wa jopo la waamuzi unaanisha kwamba Diddy anakabiliwa na kifungo cha jumla ya miaka 20 gerezani kulingana na uamuzi wa mahakama.

Share This Article