Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, ameunga mkono mswada wa marekebisho ya michezo wa mwaka 2024, akisema utafanikisha kutambua talanta miongoni mwa vijana hapa nchini.
Mswada huo uliowasilishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, unalenga kufanyia merekebisho sheria ya michezo ya sasa, ili kutoa fursa ya kubuniwa kwa hazina ya michezo ya kaunti.
Mswada huo unapendekeza kuwa kila kaunti itatenga asilimia moja ya mapato yake kwa hazina hiyo, zikiwemo ruzuku, mikopo na ufadhili kutoka kwa sekta za kibinafsi na za umma.
“Hii ni sheria bora zidi ambayo inapaswa kuungwa mkono,” alisema Seneta huyo.
“Iwapo michezo itafadhiliwa vizuri hapa nchini, inaweza changia pakubwa katika ukusanyaji wa fedha. Mataifa kadhaa yamepiga hatua kubwa kutokana na uwekezaji katika michezo.
Akitoa mfano na kaunti yake ya Vihiga ambapo hazina ya michezo hupokea chini ya shilingi milioni 10 kila mwaka, Seneta huyo alisisitiza kuwa kiasi hicho kidogo hakiwezi tekeleza mengi katika michezo.
Aidha alimtaka Seneta Sifuna kufanyia marekebisho Mswada huo, ili uruhusu serikali ya kitaifa kufadhili michezo.
“Serikali za kaunti hujenga vifaa vya michezo, lakini serikali ya kitaifa hupiga jeki micheo,’ alisema Osotsi.