Orwoba kukata rufaa kuhusu uamuzi wa mahakama

Mahakama ya kibiashara ya Milimani chini ya Hakimu Ruguru Ngotho iliamuru Orwoba amlipe karani wa Seneti fidia ya milioni 10 kwa kumharibia sifa.

Marion Bosire
2 Min Read
Gloria Orwoba - Seneta mteule

Seneta mteule wa zamani Gloria Orwoba amesema kwamba anapanga kukata rufaa kuhusu uamuzi mahakama unaomtaka alipe karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye fidia ya shilingi milioni 10 kwa kumharibia sifa.

Mahakama ya kibiashara ya Milimani chini ya Hakimu Ruguru Ngotho iligundua kuwa machapisho ya Orwoba kwenye mitandao ya kijamii yaliyomtuhumu Nyegenye kwa unyanyasaji wa kingono yalikuwa ya kumharibia sifa, yenye nia mbaya na hayakuwa na ushahidi.

Hakimu alitupilia mbali hoja ya Orwoba kwamba matamshi hayo yalilindwa na kinga ya Bunge, akieleza kuwa yalitolewa nje ya Bunge.

Mahakama ilikubaliana na Nyegenye kuwa matamshi hayo ya kumharibia sifa yalimletea msongo wa mawazo na fedheha.

“Tabia ya mshtakiwa wakati wote wa kesi hii ilikuwa ya kutojali na kutofuata masharti. Kutozwa fidia ya juu zaidi ni muhimu ili kukumbusha kwamba uhuru wa kujieleza haupaswi kutumiwa kama silaha ya kuharibu heshima ya watu” alisema Hakimu Ngotho katika uamuzi wake.

Orwoba pia aliagizwa kuomba msamaha kwa umma kupitia mitandao yake ya kijamii na katika gazeti la kitaifa ndani ya siku 30, la sivyo atozwe faini ya ziada ya Shilingi milioni moja.

Akizungumza Jumanne, Orwoba alionekana kutokata tamaa, akiahidi kupinga uamuzi huo kwa kusema:

“Nina imani na mfumo wa mahakama, ndiyo maana nimekata rufaa. Nitapinga hukumu hii” alisema Orwoba na kuongeza, “Mungu angenionea aibu ningejiuzulu… Mungu alinileta Bungeni kwa sababu maalum. Niko tayari, ninauwezo, na niko tayari kulipa gharama.”

Orwoba, ambaye alisimamishwa kwa miezi sita kabla ya kufukuzwa kutoka Bunge, alikataa wito wa kujiuzulu kufuatia uamuzi huo, akisema bado anaamini katika kesi yake.

Share This Article