Orwoba akamatwa baada ya kuziba lango la kuingia bunge

Alitaka aruhusiwe kuingia bungeni kufuatia uamuzi wa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa uliobatilisha kuondolewa kwake katika bunge la Seneti.

Marion Bosire
2 Min Read

Gloria Orwoba ambaye alikuwa akihudumu kama Seneta mteule wa chama cha UDA leo alikamatwa na maafisa wa polisi baada ya kuziba lango la kuingia bunge na gari lake.

Seneta huyo wa zamani alifika katika eneo hilo akitaka kuruhusiwa kuingia bungeni kufuatia uamuzi wa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa uliobatilisha kuondolewa kwake katika bunge la Seneti.

Walinzi katika lango hilo walimzuia kuingia hata baada yake kuwaonyesha agizo la mahakama linalomrejesha katika wadhifa wake wa awali kama Seneta Mteule.

Juhudi zake za kushawishi walinzi hao ziligonga mwamba huku walinzi wakisisitiza kwamba walikuwa wamepata maagizo kutoka kwa wakubwa wao wasimruhusu aingie.

Akizungumza nje ya majengo ya bunge, Orwoba alidhihirisha kukatishwa tamaa na matukio ya leo akilaumu bunge la Seneti kwa kukiuka sheria.

Kulingana naye, Spika Amason Kingi alikwenda kinyume na katiba kwa kuruhusu Seneta aliyeteuliwa kuchukua mahala pake kuhudhuria vikao.

Seneta huyo aliyeteuliwa maajuzi kwa jina Consolata Nabwire kulingana na Orwoba ni mgeni na hatua ya Seneti ya kuendesha kikao cha kumg’atua Gavana madarakani katika uwepo wa mgeni ni kinyume cha sheria.

Yapata wiki moja iliyopita, jopo la kusuluhisha mizozo ya vyama vya kisiasa lilielekeza chama cha UDA kufuta hatua zote ambazo kilikuwa kimechukua dhidi ya Orwoba.

Kulingana na jopo hilo, Orwoba hakupatiwa fursa ya kujitetea na kikao cha chama cha kusikiliza suala lake kilijaa makosa ya kisheria na kiutaratibu.

Share This Article